Pages

KWA MAWASILIANO ZAIDI- Email ranyikwa@yahoo.com au +255 713 257 793.

Monday, October 22, 2012

Ikulu yajitetea kauli ya Ulimboka
Na Ratifa Baranyikwa
SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Nchini, Dk. Stephen Ulimboka, kusisitiza kwamba alitekwa na mtu anayefanya kazi Ikulu, Ramadhan Ighondu, Ikulu imehamanika na kujitetea kwamba madai hayo ni ya kipuuzi.
Juzi, Dk. Ulimboka alitoa tamko akisema kwamba Ighondu ndiye aliyehusika na sakata la kuteka na kumtesa vibaya, ambalo wengine wamekuwa wakiliita jaribio la kumuua; lakini jana katika hali inayoonyesha kwamba Ikulu haiko tayari kumchukulia hatua mtumishi wake anayetuhumiwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, alisisitiza: “Ikulu iliishajibu. Tulisema haihusiki, na Rais Jakaya Kikwete amepata kuzungumza juu ya jambo hili mara nyingi.”
Wakati Ikulu ikimtetea mtuhumiwa huyo na kujaribu kujivua lawama, Jeshi la Polisi, ambalo lilimtia mbaroni raia wa Kenya na kumpeleka mahakamani kujibu tuhuma za kumteka na kumtesa daktari huyo, nalo limesita kubainisha kama litamkamata na kumhoji Ighondu, ambaye ametajwa rasmi na shahidi wa kwanza halisi katika suala hili, Dk. Ulimboka.
Badala yake maofisa wa jeshi hilo wametupiana mpira kila mmoja akidai hahusiki na suala hilo.
Katika tamko lake la kiapo lililotolewa kwa waandishi wa habari juzi, Dk. Ulimboka, kupitia kwa wakili wa kujitegemea, Nyaronyo Kicheere, alisema anamfahamu mtesaji wake, na kwamba hata akikamatwa leo hii, atakwenda kufanya utambuzi.
Alisema anashangaa kwamba polisi wameshindwa kumtia mbaroni mtuhumiwa huyo, licha ya kwamba alishatajwa na gazeti la MwanaHALISI na katika mtandao wa YouTube.
Alisema: “Nathibitisha kwamba Ramadhan Ighondu alitambulishwa kwetu kwa jina la Abeid. Binafsi ninamfahamu sana bwana huyu kwa sababu alikuwa akitumwa mara kwa mara kuja kukutana na mimi na tumekutana mara kadhaa kabla ya tukio lile.
“Nathibitisha kwamba mfanyakazi huyu wa Ikulu, ndiye aliyenipigia simu na kuniita kwenye kikao ambacho muda mfupi baadaye nilitekwa. Katika mawasiliano hayo, Abeid alikuwa anatumia simu namba 0713 760473.”
Dk. Ulimboka aliongeza kuwa anakumbuka kuwa Abeid alitambulishwa kwake na kigogo mmoja, akiwa na wawakilishi wengine wa madaktari, kuwa ndiye angehusika katika kuchukua madai na hoja za madaktari katika mgogoro kati ya madaktari na serikali.
Lakini Rweyemamu hakutaka kufafanua zaidi badala yake alisema, “Naomba uninukuu; haya madai ni upuuzi…hiki kitu kilishajibiwa.”
Alipoulizwa kama anamfahamu Ramadhan Ighondu, Rweyemamu alikwepa swali, huku akisisitiza kuwa Ikulu haihusiki naye.
Baada ya kuona swali hilo analikwepa, mwandishi alimuuliza Rweyemamu ni hatua gani ambazo Ikulu itamchukulia Ighondu kama mfanyakazi wao.
Swali hilo lilionekana kumkera Rweyemamu, akajibu kwa ukali, “Kama Ikulu haihusiki, hatuna cha kufanya juu ya jambo hilo; mnakaa mnalea maneno ya kipuuzi…Ikulu imwajibishe kuhusu nini? Haihusiki!”
Alipobanwa zaidi alisema kama kuna watu wanasema hivyo waende wakaripoti polisi.
Kauli ya jana ya Rweyemamu ni ya pili kutolewa na Ikulu kuhusu Dk. Ulimboka. Mara ya kwanza, ilipotolewa na Rais Jakaya Kikwete alipokutana na baadhi ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, akasema, “Dk. Ulimboka ana nini mpaka Ikulu imteke? Tumteke ili iweje?”
Kikwete alikwenda mbali zaidi na kusema hata Dk. Ulimboka mwenyewe alipokwenda Ikulu akiwa na viongozi wenzake alinyamaza kimya tu na kwamba waliokuwa wakizungumza ni wengine.
Hata hivyo, kwa kuwa Ikulu imesema haihusiki, na Dk. Ulimboka mwenyewe ametamka kwamba anamjua aliyemtesa, na kwamba anafanya kazi Ikulu, ni juu ya umma kuamua nani anasema ukweli.

No comments: