Pages

KWA MAWASILIANO ZAIDI- Email ranyikwa@yahoo.com au +255 713 257 793.

Monday, October 22, 2012

Kiongozi wa Uamsho aibuka, anaswa Zanzibar

•  NI SHEIKH FARID ALIYEPOTEA NA KUSABABISHA VURUGU ZA KIDINI
na Ratifa Baranyikwa

BAADA ya kupotea kwa siku nne na kusababisha vurugu kubwa visiwani Zanzibar, Kiongozi wa taasisi ya Kiislamu ya Uamsho Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed, ameonekana na kudai kuwa alitekwa nyara na polisi na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Wakati Sheikh Farid akiibuka na kudai kuwa alitekwa, serikali kwa upande wake imemkamata na kumhoji ili kubaini kama kweli alitekwa au alijificha na kusababisha uvunjifu wa amani visiwani Zanzibar.
Sheikh Farid ambaye amekuwa mwiba mkali kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), alionekana majira ya saa 2:15 usiku wa kuamkia juzi katika eneo la Mazizini, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari akiwa nyumbani kwake jana, Sheikh Farid aliibua madai mazito kwamba alitekwa nyara na polisi na maofisa wa Idara ya Usalama kwa lengo la kumhoji kuhusiana na harakati zake za kuitetea Zanzibar.
Jinsi alivyotekwa
Akisimulia jinsi alivyotekwa, Sheikh Farid alisema siku ya tukio alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni mwanafunzi wake wa Madrasa ya Mahdi Mahfoudh na kumwomba wakutane katika eneo la Mbweni, karibu na duka ambapo mbele yake kuna msikiti mdogo usiosaliwa na watu wengi.
Alisema alitoka nyumbani kwake akiwa na kijana wake mmoja ambaye hakumtaja jina na wakati huo huo alikuwa anataka kununua umeme.
Alisema alipofika sehemu ya kununulia umeme, alimwomba kijana wake akamnunulie na yeye alingia  msalani kujisaidia.
“Kitendo cha yule kijana kuondoka tu na mie kutoka msalani, nikaliona gari moja nisilolifahamu, linakuja na kuegesha mbele ya msikiti na akashuka kijana mmoja, akaniita. ‘maalim’, kisha kunitaka niingie kwenye gari na kujitambulisha kuwa yeye ni askari polisi,” Sheikh Farid alisema.
Alisema wakati askari huyo akimtaka aingie kwenye gari, ndani ya gari hilo kulikuwa na askari wengine watatu waliokuwa na silaha za moto, hivyo hakuweza kufanya ubishi wa aina yoyote.
Kwa mujibu wa Sheikh Farid, baada ya kuingia kwenye gari, waliondoka kuelekea njia ya Uwanja wa Ndege, kisha kupita ‘round about’ kama mara nne ili kumpoteza lengo, asifahamu wapi anapelekwa na kuanzia hapo hakuweza kujua anaelekea wapi hadi alipofika katika nyumba hiyo.
“Nakumbuka walikuwa watu wanne walioniteka na kuniingiza kwenye gari. Nilipofika kwenye nyumba yao, muda wote nilikuwa nimefungwa kitambaa cheusi usoni, sikuruhusiwa kutembea sehemu yoyote ndani ya nyumba hiyo na kazi yangu ilikuwa kwenda chooni kujisaidia na kwa muda wa siku tatu niliokaa sijawahi kula chakula chohote zaidi ya kunywa maji,” alisema Sheikh Farid.
Sheikh huyo alisema wakati wa mahojiano alipata vitisho ili atoe maelezo yote kuhusiana na harakati zake na masuala mengi yalikuwa yakimlenga yeye binafsi, uhusiano wake na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein na uhusiano wake na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, pamoja na safari zake za kwenda na kurudi nchini Oman.
“Watu waliokuwa wananihoji walikuwa wakitofautina, kwani kila mmoja alikuwa akitumia namna yake. Baadhi walikuwa wakali na wengine walinihoji kwa utaratibu,” alisema Sheikh Farid.
Pia alisema walichambua simu yake kuangalia aina ya watu aliokuwa akiwasiliana nao na kwamba muda wote aliokuwa ndani ya nyumba hiyo hakuwahi kula chakula cha aina yoyote, kwani hakuwa na imani nao.
Alivyoachiwa na kurejeshwa uraiani
Sheikh Farid alisema juzi wakati anarudishwa, alishushwa ndani ya gari kama mzigo kwa kusukumwa huku akiwa ameendelea fungwa kitambaa usoni na umeme ukiwa umekatika.
Alisema sehemu aliyoshushwa ndiyo ile ile iliyotumiwa na vyombo hivyo vya dola kumteka na kuondoka naye.
Mara baada ya kushushwa katika eneo hilo, alisema alikwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa mama yake eneo la Malindi ambapo alikutana na wafuasi wake wengi na kusalimiana nao, kisha akashauriwa kwenda Mbuyuni kwa mke wake mmoja ambaye anaishi eneo hilo karibu na Msikiti wa Mbuyuni.
Baada ya taarifa za kurejea kwa Sheikh Farid kuenea, mamia ya wafuasi wake walifika kwa wingi na kukaa nje ya geti la nyumba yake wakitaka kumuona kwani wengi hawakuamini kama angeachiwa akiwa hai.
Sheikh Farid aliwataka wafuasi wake watulie na wasifanye fujo huku akiwataka viongozi wa serikali kuwa waadilifu katika kushughulikia migogoro, akisema bila ya kutenda haki amani itatoweka.
“Licha ya kuniteka na kunitisha, sitarejea nyuma kamwe kuitetea Zanzibar hadi tone langu la mwisho, kwani ninachokifanya mimi na wenzangu ni kitendo kinachokubalika kisheria na hakuna wa kutuzuia,” alisema Sheikh Farid.
Alisisitiza kuwa wataitetea Zanzibar hadi iwe na dola na mamlaka kamili  na irudi katika hadhi yake kama ilivyokuwa mwaka  1963.
Waziri Nchimbi atoa kauli nzito
Katika hatua nyingine, serikali imesema kuwa inachunguza tukio la kutoweka na kurejea kwa Sheikh Farid na kusababisha vurugu na mauaji visiwani Zanzibar.
Tayari Jeshi la Polisi jana lilimhoji kwa saa kadhaa ili kubaini kama alijificha au alitekwa nyara kama anavyodai.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Akizungumzia tukio hilo, Dk. Nchimbi alisema polisi walipata taarifa za kuonekana kwa Sheikh Farid jana asubuhi katika eneo la Mji Mkongwe.
Alisema Sheikh Farid alikuwa akihojiwa na polisi katika Kituo cha Mademwa jana ili kueleza mahali alikokuwa.
Wakati Dk. Nchimbi akieleza hayo, taarifa nyingine zinasema kuwa Sheikh Farid alijificha kwa makusudi ili kuleta vurugu.
Dk. Nchimbi alisema ikithibitika kwamba alijificha kwa makusudi ni kosa kisheria, kwa sababu kutoweka kwake kulisababisha uvunjifu wa amani.
Alisema kutoweka kwa Sheikh Farid Oktoba 16 mwaka huu Zanzibar kulisababisha vurugu na mauaji ya askari polisi, Koplo Said Abraham Juma, aliyeuawa kwa kukatwa mapanga Oktoba 18, mwaka huu.
Akizungumzia vurugu zilizotokea jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa zilizotokana na kukamatwa kwa Sheikh Ponda Issa Ponda, Dk. Nchimbi alisema kuanzia sasa serikali haitawavumilia wanaofadhili, wanaowatuma na wanaofanikisha vurugu hizo.
Alisema wanafanya uchunguzi kubaini kama kuna watu wanaowezesha maandamano ya Waislamu, kwa sababu wamegundua kuwa watu hao wamekuwa wanatumia magari na vipaza sauti kuzunguka mitaani ambavyo vinahitaji fedha.
Kuhusu tukio lililotokea Ijumaa alisema baada ya upelelezi serikali imebaini kuwa wafuasi wa Sheikh Ponda walijaribu kuwashawishi watu waende Ikulu ama sehemu nyingine kushinikiza kiongozi wao aachiliwe.
“Mahakama haijampa dhamana, hivyo kujaribu kushinikiza atolewe ni kosa kisheria na wanaingilia uhuru wa mahakama,” alisema Dk. Nchimbi.
Nchimbi alisema hakuna vurugu ama maandamano yatakayosaidia Ponda na wenzake watoke mahakamani.
Nchimbi pia ametangaza kusitisha mihadhara yote ya kidini nchi nzima kwa siku 30 mpaka hapo watakapoona namna bora ya kufanyika.
“Kuna watu ambao wanafikiri hawaguswi, wanasema wakiguswa moto utawaka, sisi tumekataa, kama moto ukiwaka uwake tutauzima…mkiandamana tunawakung’uta,” alisisitiza Dk. Nchimbi.
Aliongeza kuwa: “Tunakoelekea siko, tunaanza kutazamana kwa misingi ya kidini, kushabikia mpasuko wa kidini…sasa hivi kama kuna mtu amesikiliza hivi vyombo vya habari vya kimataifa…wanatoa taarifa kwa watalii wao wanaokuja huku kwamba Tanzania iko kwenye mpasuko wa kidini.
“Tunapelekwa sehemu ambayo watu wataacha kusalimiana, kupendana, tunajua athari za chokochoko za kidini, wenzetu Ulaya wanalifahamu hili vizuri ndiyo maana leo hii ni waangalifu sana, miaka 400 iliyopita watu milioni nne walikufa, Sudan watu karibu milioni mbili, Lebanon hadi waliposema sasa tukae tuzungumze, walikuwa wamepoteza maisha ya watu 250,000,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Nchimbi, nchi yetu haitaki kufika huko na katika hilo alisisitiza serikali inakaribisha mazungumzo yasiyo ya vitisho na viongozi wa dini zote katika kujenga amani na utulivu wa nchi yetu.
Alisema serikali inawataka Watanzania kuheshimu dini za watu wengine na kwamba kudharau vitu vya ibada, kama kuharibu vitabu vya dini kama Kurani au Biblia, kushambulia waumini au majengo ya ibada ya dini nyingine ni kosa kisheria na havitavumiliwa.

No comments: