Pages

KWA MAWASILIANO ZAIDI- Email ranyikwa@yahoo.com au +255 713 257 793.

Wednesday, October 24, 2012

Waziri Mulugo aiaibisha serikali

• Asema Tanzania ni Muungano wa Zimbabwe, Pemba na Tanganyika
 
na George Maziku



NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, amemwaibisha Rais Jakaya Kikwete na taifa kwa ujumla mbele ya jamii ya kimataifa, baada ya kuitangazia dunia kuwa Tanzania imetokana na muungano wa visiwa vya Zimbabwe na Pemba vilivyoungana na Tanganyika.
Mbali na hilo, aliwaambia mamia ya wajumbe kutoka mataifa mbalimbali katika Bara la Afrika kuwa, Tanzania ilizaliwa mwaka 11964.
"Wasilisho langu litakuwa na sehemu saba…Utangulizi, Tanzania iliundwa mwaka 11964 kwa kuunganisha visiwa vya Bahari ya Hindi vya Zimbabwe na Pemba vilivyoungana na nchi ya Bara iliyokuwa ikiitwa Tanganyika…," alisema Naibu Waziri Mulugo kwa kujiamini na bila kuonyesha dalili yoyote kuwa alikuwa amekosea.
Naibu waziri huyo alikuwa akiwasilisha mada katika mkutano wa viongozi na wataalamu wa elimu katika Bara la Afrika, ambao ulifanyika Afrika Kusini kuanzia Oktoba 5-7, mwaka huu.
Kuboronga huko kwa naibu waziri huyo kumeibua mjadala mkubwa na mzito miongoni mwa Watanzania wa kada na rika mbalimbali, huku wengi wakianza kupata wasiwasi juu ya uwezo wa watu wanaoteuliwa na Rais Kikwete kushika nyadhifa mbalimbali serikalini.
Watu wengi waliotoa maoni yao juu ya suala hili kupitia mitandao ya kijamii ya Jamii Forum, Wanabidii, Facebook na Twiter wameonyesha wasiwasi mkubwa na kiwango cha elimu na weledi wa Mulugo na kuuliza swali; "elimu ya waziri huyu inatosheleza kumudu majukumu yake ya Naibu Waziri wa Elimu?"
Wasifu wa Naibu Waziri Mulugo uliopatikana kupitia mtandao wa Google, unaonyesha kuwa ana elimu ya shahada ya kwanza aliyoipata kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, kati ya mwaka 2002 na 2008.
Anadai katika wasifu huo kuwa kabla ya kuingia chuo kikuu, amesoma katika shule za sekondari za Songea Boys High School kwa masomo ya kidato cha tano na sita kuanzia mwaka 1994 mpaka 1996, na Sekondari ya Mbeya kwa masomo ya kidato cha kwanza mpaka cha nne kuanzia mwaka 1990 mpaka 1993.
Mulugo amejieleza kuwa kati ya mwaka 2000 na 2004 alifanya kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari Southern Highland, huku akiwa hajapata mafunzo yoyote ya taaluma ya ualimu.
Alipotafutwa kwa njia ya simu kufafanua alivyojieleza, Waziri Mulugo alisema alikuwa mjini Dodoma kuhudhuria kikao cha Baraza la Mawaziri, hivyo hakuwa na muda wa kuzungumza na gazeti hili.
 
 
 
Source; Tanzania Daima

No comments: